Wanafunzi, watenda kazi wahimizwa kushirikiana kudumisha usafi shuleni
31 August 2026, 17:42

Mwalimu Michael anasisitiza kuwa jukumu la kutunza mazingira jukumu la wahudumu wa usafi pekee. Bali wanafunzi, walimu na uongozi wa shule au chuo wanapaswa kushirikiana kuhakikisha taka zinatupwa sehemu husika, vyoo vinatunzwa na maeneo ya kujifunzia yanabaki safi kila siku.
Na Crispine Gerald.
Usafi katika mazingira ya shule na vyuo ni jambo muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira salama na rafiki kwa kujifunza.
Usafi huo unahusisha hali ya vyoo, upatikanaji wa maji, sehemu za kunawa mikono, utunzaji wa taka pamoja na usafi wa madarasa na maeneo ya pamoja.
Kwa mujibu wa UNICEF huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi, maarufu kama WASH, ni muhimu kwa afya, ustawi na maendeleo ya wanafunzi, Tathmini ya kitaifa ya WASH shuleni pia imeonyesha kuwa bado kuna changamoto katika upatikanaji na utunzaji wa huduma za usafi katika baadhi ya shule nchini.
Baadhi ya wanafunzi wanaeleza hali ya usafi katika shule au vyuo vyao, wakitaja maeneo wanayoona yanafanyiwa usafi vizuri pamoja na maeneo ambayo bado yanahitaji maboresho zaidi ya usafi
Michael Emmanuel ni mwalimu wa shule ya Msingi Makole jijini Dodoma amesema usafi wa mazingira ni sehemu muhimu ya kujenga mazingira bora ya kujifunzia, pi usafi haupaswi kuishia kwenye kufagia pekee, bali unapaswa kujumuisha vyoo safi, maji ya kutosha, sehemu za kunawia mikono na utunzaji sahihi wa taka.