Wanawake watakiwa kutambua haki yao ya umiliki wa ardhi
8 September 2026, 17:11

Mila na mitazamo potofu haipaswi kuwa sababu ya kuwanyima wanawake haki ya kumiliki mali, akisisitiza umuhimu wa jamii kutoa elimu kuhusu haki za wanawake na kuhakikisha wanapata nyaraka halali za kuthibitisha umiliki wao.
Na Daniel Njau.
Wananchi, hususan wanawake, wamehimizwa kutumia haki yao ya kisheria kumiliki ardhi na mali nyingine, huku jamii ikitakiwa kuachana na mila na desturi potofu zinazowazuia wanawake kupata haki yao ya umiliki.
Baadhi ya wananchi wamesema mila na desturi katika baadhi ya maeneo, hasa vijijini, zimekuwa changamoto kwa wanawake kumiliki mali, hali inayowafanya kukosa haki zao stahiki.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mwanasheria kutoka TAWLA Tawi la Dodoma, Lilian Mmbwana, amesema kila mtu ana haki ya kumiliki ardhi na kupata nyaraka halali za umiliki, ikiwemo hati ya eneo husika, huku mwanamke akiwa na haki sawa na mwanaume katika kumiliki na kutumia ardhi kwa mujibu wa sheria.