Dodoma FM

SUA yaibua teknolojia ya panya kubaini mabomu

31 August 2026, 17:20

Makamu mkuu wa SUA, Profesa Rafael Chibunda, amesema ushirikiano huo umeanzishwa kwa misingi ya kibinadamu. Picha na Anwary Shabani.

Hatua hiyo inaendelea kuonyesha namna tafiti na ubunifu wa kisayansi vinavyoweza kutumika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususani katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro na mabomu ya ardhini.

Anwar Shabani.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo – SUA, kwa kushirikiana na taasisi ya APOPO wameanzisha program ya kutumia panya waliofunzwa maalum kwa ajili ya kubaini maeneo yenye mabomu  na kuyaondoa kwa usalama.

Akizungumza katika ofisi za Habari Maelezo, Mtumba jijini Dodoma, Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Rafael Chibunda, amesema ushirikiano huo umeanzishwa kwa misingi ya kibinadamu, kutokana na madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na mabomu ya ardhini kwa wananchi wanaorejea katika maeneo yao baada ya migogoro.

Profesa Chibunda amesema SUA haitoi huduma hiyo kwa lengo la kupata fedha kutoka kwa nchi zinazokabiliwa na changamoto ya mabomu ya ardhini, bali inalenga kusaidia jamii zilizo katika mazingira hatarishi, akieleza kuwa panya hao wamewahi kufanya kazi hiyo kwa mafanikio nchini Msumbiji pamoja na Angola

Aidha, amesema zaidi ya asilimia 90 ya miradi ya utafiti inayotekelezwa na SUA hufanyika kwa kushirikiana na jamii, kwa lengo la kupeleka teknolojia mpya pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu unaoweza kuboresha shughuli wanazofanya tayari.

Sauti na Anwary Shabani.