Dodoma FM

Serikali yaendele kuhimiza chanjo ya polio kwa watoto

28 August 2026, 16:22

Kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha afya na ustawi wa watoto nchini.Picha na Anwary Shabani.

Na Anwary Shabani.

Zoezi la utoaji chanjo ya Polio linatarajiwa kuendelea hadi Agosti 30, 2026, likihusisha jamii kwa ujumla, hususani wazazi na walezi, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto aliyelengwa anapata chanjo.

Serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kuilinda Tanzania dhidi ya ugonjwa wa Polio kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo, licha ya nchi kutokuwa na mgonjwa wa Polio kwa sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, amesema hayo wakati akifungua rasmi kampeni ya utoaji chanjo ya Polio katika Shule ya Msingi Nkuhungu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alhaj Shekimweri amesema kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha afya na ustawi wa watoto nchini, akieleza kuwa watoto wameendelea kuwa sehemu muhimu ya programu mbalimbali za afya zinazotekelezwa na Serikali.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kinga dhidi ya Polio, ikiwemo kuwafikia watoto kwa chanjo, ili kuzuia uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini au kuenea endapo utatokea katika maeneo mengine.

Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Rosmith Mkoko, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo hiyo, huku akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo kwa wakati.

Katika kampeni hiyo, Wilaya ya Dodoma imelenga kuwafikia jumla ya watoto Laki mbili na elfu saba, tisini na sita ikiwa ni sehemu ya watoto milioni moja, elfutatu na sitini na moja. wanaolengwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dodoma.

Sauti na Anwary Shabani.