Wanawake watakiwa kuadhimisha ‘birthday’ kwa kupima saratani ya kizazi, matiti
7 September 2026, 16:56

Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Mariam Mungula Foundation, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Mungula, amesema taasisi hiyo inalenga kutoa elimu na kuongeza uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa wanawake, ikiwemo afya ya homoni, ukomo wa hedhi, afya ya akili, saratani ya mlango wa kizazi, VVU, pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi na ujasiriamali.
Na Elizabeth Mwinuka.
Wanawake wametakiwa kujali afya zao kwa kupima mara kwa mara, hususan saratani ya mlango wa kizazi na matiti, ili kubaini magonjwa mapema na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kupata matibabu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati akizindua Taasisi ya Mariam Mungula Foundation inayojihusisha na masuala ya afya ya wanawake.
Dkt. Samizi amewataka wanawake kuanza kupima afya zao wanapofikisha miaka 35 na kuendelea kufanya uchunguzi huo kila mwaka, akisisitiza kuwa afya inapaswa kuwa sehemu ya sherehe zao za maisha na kuhakikisha afya ya mlango wa kizazi na matiti iko salama kabla ya kusherehekea siku zao za kuzaliwa.