Dodoma FM
Dodoma FM
3 Machi 2026, 12:50

Amesema kauli mbiu ya “Keroyako, wajibuwangu” imeboreshwa na sasa KAULI MBIU NI KERO YAKO,WAJIBU WANGU,TABASAMU NA DKT SAMIA ili kuendana na dhamira ya Serikali ya kuona Watanzania wanapata furaha na huduma bora.
Na Ibrahim Jamal.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametangaza rasmi kuanza kwa kikao maalum cha siku tatu chenye lengo la kutatua kero mbalimbali za wananchi pamoja na kutoa huduma za kijamii bure.
Akizungumza na wanahabari, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kikao hicho kitafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 6 Machi 2026 katika viwanja vya Nyerere Square.
Amesema zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na maelekezo ya viongozi wengine wa Serikali, akiwemo Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Riziki Shemdoe.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, shughuli hizo zitajikita katika mambo matatu makuu
Kusikiliza na kutatua kero za wananchi ambapo taasisi zote za umma mkoani Dodoma zitakuwepo kutoa huduma papo kwa papo.
Mwananchi mwenye changamoto ya barabara, maji, umeme, bima ya afya au masuala ya halmashauri atapata huduma katika eneo moja bila kuzungushwa.
Sambamba na hayo wananchi watapata fursa ya kupewa taarifa kuhusu mafanikio ya Serikali ndani ya siku mia moja mkoani Dodoma, pamoja na mipango ya maendeleo inayo tekelezwa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesema mkoa unaandaa mfumo maalum wa kupokea, kusikiliza na kufuatilia kero kuanzia ngazi ya kitongoji hadi mkoa, huku taarifa za utekelezaji zikitolewa kila mwezi ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.