Ujenzi wa daraja waleta tumaini kwa wananchi Nzali
17 August 2026, 17:22

Kukamilika kwa daraja hilo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha usafiri na usalama wa wananchi, huku likitoa fursa zaidi kwa shughuli za kilimo, biashara na huduma za kijamii katika maeneo hayo.
Na Anwary Shaban.
Baada ya adha ya muda mrefu pamoja na maafa mbalimbali yaliyotokana na ukosefu wa daraja katika kijiji cha Nzali wilayani Chamwino hatimaye wakazi wa kijiji hicho wamepata tumaini baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja.
Kwa mujibu wa wananchi hao kijiji cha Nzali kwa muda mrefu kilikabiliwa na kukatika kwa mawasiliano marakwamara hasa msimu wa mvua kutokana na korogo kukatisha katika barabara na kupelekea huduma za usafiri kukatishwa huku baadhi ya wananchi wakipoteza maisha kwa kusombwa na maji wakati wa mvua.
Wakazi hao wanasema kukamilika kwa daraja hilo kumekuwa suluhisho la changamoto iliyodumu kwa muda mrefu, huku likiwawezesha kusafiri kwa usalama nakuimarisha mawasiliano kati ya Kijiji cha Nzali, Chilonwa hadi Itiso.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi.Janeth Manyanja, amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 14, akiwataka wananchi kulitunza na kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Daraja la Nzali lina urefu wa mita 60, huku likiambatana na kilomita 1.5 za barabara ambazo zimekuwa kiungo muhimu katika kurahisisha usafiri kutoka Chamwino, Dabalo, Chilonwa hadi Itiso na hatimaye kuunganisha na barabara kuu ya Dodoma–Arusha.