Dodoma FM

Wananchi watakiwa kuwatilia shaka raia wanaoishi nchini kinyume cha sheria

15 September 2026, 15:08

Picha ni wananchi walio ya kimbia makaazi yao na kuelekea nchi nyingine kujihifadhi. Picha na DW Idhaa ya kiswahili.

Kampeni ya Mjue Jirani Yako inaendelea kuhamasisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola, kwa lengo la kuhakikisha taarifa muhimu za kiusalama zinawasilishwa kwa wakati na hivyo kusaidia kujenga jamii yenye ulinzi na usalama.

Na Anwary Shabani.

Wito umetolewa kwa wananchi kuwa macho na wageni wanaoingia na kuishi katika maeneo yao, huku wakihimizwa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapobaini uwepo wa watu wanaowatilia shaka au wanaoishi nchini kinyume cha sheria.

Wito huo umetolewa na Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji kutoka Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Joseph Mgoba, wakati akiendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kampeni ya “Mjue Jirani Yako”, inayolenga kuimarisha usalama na ulinzi katika jamii.

Mgoba amesema kampeni hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa umuhimu wa kuwafahamu watu wanaoishi katika maeneo yao, hususan wageni, na kutoa taarifa kwa Polisi, Uhamiaji au Ofisi ya Mtendaji pale wanapobaini viashiria vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mwatano, Dodoma, wameeleza kuwa uwepo wa wahamiaji wanaoingia na kuishi nchini kinyume cha sheria unaweza kuleta changamoto mbalimbali katika jamii, hivyo wametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Uhamiaji na mamlaka nyingine husika.

Akifafanua zaidi, Mgoba amesema mwananchi anaweza kutoa taarifa katika eneo lililo karibu naye, ikiwemo kituo cha Polisi, Ofisi ya Uhamiaji ya Wilaya au sehemu nyingine rasmi zinazopokea taarifa za kiusalama, ili mamlaka ziweze kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki.

Simulizi na Anwary Shabani.