Dodoma FM

Wananchi waomba maboresho ya barabara na madaraja Dabalo

6 October 2026, 17:46

Pichani ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara zinazohitaji marekebisho. Picha na mwananchi.

Wananchi wa vijiji vya Manyemba na Chiwondo, Kata ya Dabalo, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara, hususan madaraja, ambayo imekuwa ikiwapa changamoto na kukata mawasiliano wakati wa msimu wa mvua.

Na Victory Chigwada.

Wakizungumza kuhusu changamoto hiyo, wananchi hao wamesema mvua zinaponyesha maji hujaa katika baadhi ya madaraja na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya vijiji hivyo, hali inayowafanya kushindwa kupata baadhi ya huduma muhimu.

Wameongeza kuwa hali hiyo huathiri zaidi wagonjwa wanaohitaji kufikishwa katika vituo vya afya, pamoja na shughuli za usafirishaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Dabalo, Omary Kiguna, amesema licha ya baadhi ya maeneo ya barabara kupitika vizuri, bado kuna changamoto katika maeneo mengine zinazohitaji hatua za Serikali, ikiwemo maeneo yanayohudumia vijiji vya Manyemba na Chiwondo.

Simulizi na Victory Chigwada.