Dodoma FM

Wakazi wa Igandu wameomba kukamilishwa kwa jengo la mama na mtoto

26 October 2026, 17:25

Picha ni ujenzi wa jengo la mama na mtoto ukiendelea. Picha kutoka facebook.

Upatikanaji wa huduma bora za afya ya mama na mtoto ni muhimu katika kulinda maisha ya wajawazito na watoto wachanga, hasa wakati wa ujauzito na kujifungua. Hata hivyo, kutokuwepo kwa miundombinu ya kutosha katika baadhi ya maeneo ya vijijini kunaweza kuongeza ugumu wa kupata huduma hizo kwa wakati, huku baadhi ya wajawazito wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa Kitongoji cha Ndugai, Kijiji cha Igandu, wameiomba Serikali kuharakisha ukamilishaji wa jengo la mama na mtoto ili kuboresha huduma kwa wajawazito na kupunguza hatari ya baadhi ya wanawake kujifungua njiani wanapolazimika kusafiri kutafuta huduma za afya katika maeneo jirani.

Wamesema kutokamilika kwa jengo hilo kunawalazimu wajawazito kutumia wodi moja na wagonjwa wengine, hali inayosababisha usumbufu na wakati mwingine kuwafanya kusafiri kwenda vituo vya afya vya mbali wanapohitaji kujifungua.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igandu, Joyce Chiloweka, amekiri kuwepo kwa changamoto za huduma za afya kijijini hapo, zikiwemo uhaba wa watumishi na kutokamilika kwa jengo la mama na mtoto.

Chiloweka amesema wananchi walianzisha ujenzi wa jengo hilo na baadaye kulikabidhi kwa Serikali kwa ajili ya umaliziaji, huku akieleza kuwa tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.

Simulizi na Victory Chigwada.