Shigela awataka wanachama wa vyama vya ushirika kutumia kliniki ya ushirika.
1 October 2026, 17:19

Kliniki hiyo inalenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazokabili vyama vya ushirika, pamoja na kutoa elimu kuhusu uendeshaji bora wa vyama na namna ya kukabiliana na migogoro.
Na Hamis Kitana.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Martin Shigela, amewataka wanachama wa vyama vya ushirika kutumia fursa ya Kliniki ya Ushirika kupata elimu na kueleza changamoto zinazokabili vyama vyao ili zipatiwe ufumbuzi.
Shigela ametoa kauli hiyo baada ya kutembelewa ofisini kwake na Naibu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika chini, Consolatha Kiluma, wakati Kliniki ya Ushirika ikiendelea kwa siku tatu wilayani Babati.
Katika kliniki hiyo, baadhi ya wanachama wameiomba Serikali kuondoa mfumo wa ukusanyaji wa mazao kupitia Aggregators, wakidai kuwa mfumo huo unawafanya wakulima kuuza mazao kwa bei wanayoieleza kuwa ya chini. Pia wamependekeza mamlaka ya ukusanyaji irejeshwe kwa vyama vya ushirika ili wanachama wanufaike zaidi.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika RIVACU, Peter Yuda, pamoja na Mjumbe wa Chama cha Ushirika Ordoy Babati, Ahmed Athuman, wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika mfumo huo.
Kwa upande wake, Naibu Mrajis wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Consolatha Kiluma, amesema kliniki hiyo inalenga kuwafikia wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika, kuwapa elimu na kusaidia kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya vyama hivyo.