Wazee watakiwa kurejea katika nafasi ya kujenga maadili
1 October 2026, 16:59

Itakumbukwe kuwa kila octoba mosi ni siku ya wazee duniani licha ya kukua kwa tecknolojia na utandawazi bado tunapaswa kuwachukulia wazee kama tunu na kutumia busara zao na maarifa kujenga na kuendeleza mambo mbalimbali.
Na Daniel Njau.
Katika jamii ambayo maadili yanaonekana kukabiliwa na changamoto mbalimbali, baadhi ya vijana wameeleza kuwa wazee wanapaswa kurejea katika nafasi yao ya kuwa chachu, walezi na walimu wa kizazi kipya, kwa kutumia uzoefu wao katika kusimamia maadili na kutoa mwongozo kwa jamii.
Vijana hao wanasema kwa sasa baadhi ya wazee wameonekana kutokuwa na msimamo katika kukemea tabia zinazoweza kuathiri maadili ya jamii, huku wengine wakieleza kuwa mabadiliko ya teknolojia na utandawazi yamefanya baadhi ya wazee kuishi kwa mtindo unaofanana na vijana, hali inayodaiwa kupunguza nafasi yao kama waelekezi wa kizazi kinachokua.
Kwa upande wake, Rafael Mchea, mzazi na babu wa wajukuu, anasema changamoto nyingine ni baadhi ya vijana kutokuwa tayari kusikiliza ushauri wa wazee, wakiamini kuwa wanaweza kufanya maamuzi yao wenyewe bila mwongozo wa waliowatangulia.
Anasisitiza kuwa ili kujenga jamii yenye maadili, wazee wanapaswa kusimama katika nafasi zao, huku vijana nao wakitambua thamani ya uzoefu na ushauri wa kizazi kilichowatangulia.
Hata hivyo, katika dunia inayobadilika kwa kasi kutokana na teknolojia na utandawazi, je, tatizo la mmomonyoko wa maadili linapaswa kubebwa na wazee pekee, au ni wakati wa vijana na wazee kukaa pamoja na kujenga upya misingi ya jamii?