Wananchi Mpwapwa waomba ongezeko la walimu liendane na miundombinu iliyopo
8 October 2026, 17:01

Jamii wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma imeipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya shule, huku ikiomba uwekezaji huo uende sambamba na ongezeko la walimu ili wanafunzi wapate elimu katika mazingira bora.
Na Steven Noel.
Wakizungumza na Dodoma FM katika mahojiano maalumu yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali wilayani humo, baadhi ya wakazi wamesema Serikali imepiga hatua katika ujenzi na uboreshaji wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
Hata hivyo, wamesema bado kuna changamoto ya upungufu wa walimu katika baadhi ya shule, hali inayowalazimu wananchi katika baadhi ya vijiji kuwakodi walimu wa kujitolea ili kusaidia kupunguza uhaba huo.
Wamesema ongezeko la walimu ni muhimu ili uwekezaji unaofanyika katika miundombinu ya shule uendane na upatikanaji wa huduma bora ya elimu kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kingiti amesema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule unapaswa kuzingatia pia mahitaji maalumu ya watoto wa kike, ikiwemo uwepo wa vyoo salama, vyenye faragha na mazingira yanayowawezesha kuendelea na masomo wakati wa hedhi.