Uelewa wa sheria za kazi wasisitizwa kulinda haki za mwajiri, mwajiriwa
15 October 2026, 16:15

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 inaweka misingi ya kusimamia haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi. Utekelezaji wa sheria hiyo ni muhimu katika kuzuia unyonyaji, kulinda wafanyakazi dhidi ya kusitishiwa ajira bila kufuata taratibu za haki, na kuwawezesha waajiri kusimamia nidhamu na ufanisi kwa kuzingatia sheria.
Na Husna Munisi
Uelewa wa sheria za kazi ni muhimu katika kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kujenga mazingira bora ya ajira na kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika maeneo ya kazi.
Sheria za kazi nchini Tanzania zinaweka utaratibu wa kusimamia uhusiano kati ya mwajiri na mwajiriwa, ikiwemo mikataba ya ajira, malipo ya mishahara, muda wa kazi, likizo, nidhamu na taratibu za kusitisha ajira.
Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria Onesmo Daudi kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), amesema waajiri wana wajibu wa kuhakikisha masharti ya ajira yanazingatia sheria zilizopo na haki za wafanyakazi zinalindwa.
Daudi ameongeza kuwa ni muhimu masharti ya ajira kuwekwa wazi, wafanyakazi kulipwa ujira unaostahili, kuzingatiwa kwa muda wa kazi na mapumziko, pamoja na kutolewa kwa likizo na stahiki nyingine kwa mujibu wa sheria.