Wazazi wametakiwa kushiriki katika maendeleo ya elimu
9 October 2026, 16:26

Ushiriki wa wazazi katika malezi, mazungumzo na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto umetajwa kuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayowasaidia kufikia malengo yao kielimu. Hivyo, wazazi, walimu na jamii wametakiwa kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Na Daniel Njau.
Baadhi ya wananchi wamesema wanawake wamekuwa wakishiriki zaidi katika kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni ikilinganishwa na wanaume. Wamesema baadhi ya wazazi hushindwa kutekeleza wajibu huo kutokana na ukosefu wa elimu, majukumu mengi na uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.
Akizungumzia suala hilo, mshauri wa malezi na familia, Bi. Magdalena Mtiku, amesema elimu ya mtoto ni jukumu linalohitaji ushiriki wa wadau mbalimbali, huku wazazi wakiwa na nafasi ya msingi katika malezi, uelekezaji na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto wao.
Ameeleza kuwa changamoto zinazoweza kuathiri maendeleo ya watoto kielimu ni pamoja na ushawishi wa makundi rika, umaskini na mimba za utotoni. Kwa upande mwingine, baadhi ya wananchi wamesema mafanikio ya mwanafunzi yanategemea pia utayari wake wa kujifunza na bidii katika masomo.
Hivyo, wazazi wametakiwa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu kama chakula, mavazi na malezi bora, huku wakipanga majukumu ya familia kwa namna inayowapa muda wa kutosha wa kujisomea na kufanya vizuri katika masomo yao.