Dodoma FM

Shule ya sekondari Mtumba yaomba msaada wa huduma ya maji

2 October 2026, 16:29

Picha ni maji safi kutoka vyanzo vya idara ya maji ,japo kuna changaoto ya majai katika shule sekondari mtumba. Picha na Dodoma fm.

Wanafunzi 134 wanatarajiwa kuhitimu kidato cha nne katika shule hiyo. Takwimu za matokeo ya miaka mitatu iliyopita zinaonesha wastani wa ufaulu kwa kutumia GPA ulikuwa 4.1445 mwaka 2023, 3.8144 mwaka 2024 na 3.9755 mwaka 2025.

Na Victory Chigwada.

Shule ya Sekondari Mtumba jijini Dodoma imeeleza kuwa ukosefu wa huduma ya maji ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili shule hiyo, hali inayowalazimu wanafunzi kutumia muda wa ziada kutafuta huduma hiyo.

Akizungumza katika mahafali ya 19 yaliyofanyika shuleni hapo, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Godfrey Mseti, amesema ukosefu wa maji ni moja ya changamoto kubwa inayokwamisha mazingira bora ya kujifunzia.

Mseti amesema licha ya juhudi zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Antony Mavunde, bado hakuna mafanikio yaliyopatikana, hivyo amewataka wadau kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma ya maji inafikishwa shuleni hapo.

Baadhi ya wazazi wa Mtumba wamesema ukosefu wa maji ni adha kwa wanafunzi, kwa kuwa huwalazimu kutumia muda wa masomo kutafuta huduma hiyo, hali inayoweza kuathiri ujifunzaji wao.

Kwa upande mwingine, Mwalimu Mseti amewataka wanafunzi wanaotarajia kuhitimu kidato cha nne shuleni hapo kuwa na maadili, nidhamu, bidii na uadilifu, pamoja na kutumia maarifa waliyopata katika kujenga maisha yao ya baadaye.

Simulizi na Victory Chigwada.