Dodoma FM

Ukosefu wa huduma za kilimo, mifugo changamoto Mbelezungu

16 November 2026, 16:46

Picha ni mifugo aina ya ng’ombe wakiwa katika malisho. Picha na Michuzi Blog.

Wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mbelezungu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma muhimu za kilimo na mifugo, hali inayochangia uzalishaji hafifu wa mazao pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yanayoathiri mifugo yao.

Na Victor Chigwada.

Wakizungumza na Taswira ya Habari, wakazi wa eneo hilo wamesema wakati wa msimu wa mvua mifugo hushambuliwa zaidi na magonjwa, huku kukosekana kwa josho la kuogeshea mifugo na maduka ya pembejeo za mifugo kukiwafanya washindwe kupata huduma muhimu za kinga na matibabu kwa wakati, hali inayosababisha baadhi ya mifugo kufa.

Aidha, wananchi hao wamesema ukosefu wa pembejeo za kilimo unawalazimu kuendelea kufanya kilimo cha kienyeji, hali inayochangia kupatikana kwa mavuno hafifu na kuathiri kipato chao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, George Isaya, amekiri kuwepo kwa changamoto hizo, akieleza kuwa wakulima na wafugaji wanahitaji kupatiwa huduma za pembejeo za kilimo na mifugo pamoja na kujengewa josho ili kuboresha shughuli zao za uzalishaji. Ameomba serikali kuingilia kati na kusaidia upatikanaji wa huduma hizo kijijini hapo.

Isaya ameongeza kuwa uhaba wa wataalamu wa kilimo na mifugo ni changamoto nyingine inayowakabili wakazi hao, akisema wanalazimika kumtegemea Afisa Mifugo wa Kata ya Majeleko, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma za kitaalamu pale mifugo inapougua.

Amesema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wafugaji kujichukulia jukumu la kutibu mifugo yao bila kuwa na ujuzi wa kitaalamu, jambo linaloweza kuhatarisha afya ya mifugo na kuathiri uzalishaji.

Simulizi na Victory Chigwada.