Dodoma FM

Vijana Matumbulu waridhishwa na mradi wa AHADI

27 November 2026, 15:56

Wamesema mradi huo utasaidia wananchi kupata elimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili.Picha na Anwary Shaban.

Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia hufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka, yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Na Bennard Komba.

Vijana katika Kata ya Matumbulu, Jijini Dodoma, wameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa AHADI unaotekelezwa na Shirika la TAHEA kwa kushirikiana na World Vision, unaolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Wakizungumza na Dodoma FM baada ya kushiriki mdahalo uliofanyika katika Mtaa wa Muungano, wamesema mradi huo utasaidia wananchi kupata elimu kuhusu aina mbalimbali za ukatili, namna ya kujikinga na mahali sahihi pa kutoa taarifa za vitendo hivyo.

Diwani wa Kata ya Matumbulu, Godfrey Gideon, amezipongeza TAHEA na World Vision kwa kuifikishia jamii elimu hiyo, akieleza kuwa ni mchango muhimu katika kujenga kizazi chenye uelewa na jamii isiyovumilia vitendo vya ukatili. Pia amewahimiza wadau wengine kujitokeza kushirikiana katika kutoa elimu kwa wananchi.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aneth Mwambia, amesema mdahalo huo unaonesha juhudi za Serikali katika kuongeza uelewa wa wananchi ili waweze kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika kupinga ukatili.

Naye Msimamizi wa Mradi wa AHADI, Frolence Seme, amesema mdahalo huo ulilenga kuibua changamoto zinazochangia vitendo vya ukatili katika jamii na kujadili suluhisho zitakazosaidia kujenga jamii yenye amani na usawa.

Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia hufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kila mwaka, yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Kaulimbiu ya mwaka huu “Tuungane Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, Jenga Taifa Imara Lenye Haki na Usawa Kuelekea Dira 2050.”

Ripoti ya Mariam Kasawa.