Wananchi Kondoa mji kunufaika na huduma ya klinik ya ardhi
22 October 2026, 11:46

Hatua hiyo inaweka fursa muhimu kwa wakazi wa Kondoa Mji kurahisisha upatikanaji wa hati za ardhi, kupunguza gharama za ufuatiliaji na kuimarisha uthibitisho wa umiliki halali wa viwanja vyao.
Na Anwary Shaban.
Wananchi wilayani Kondoa wameanza kunufaika na huduma za kliniki ya ardhi wilayani hapo , hatua inayolenga kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri hadi jijini Dodoma kufuatilia hati za viwanja vyao.
Kliniki hiyo inayoendeshwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi na viongozi wa Halmashauri ya Mji Kondoa, inafanyika katika viwanja vya ofisi za halmashauri hiyo na inalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za ardhi kwa urahisi na kwa muda mfupi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Bi.Happiness Mtutwa, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata hati za viwanja vyao, amesema Kondoa Mji ina zaidi ya viwanja 3,000 vilivyopimwa, lakini wamiliki wenye hati za viwanja hivyo ni chini ya 100.
Kwa upande wake, mmoja wa wananchi waliofaidika na huduma hiyo, Issa Mgange, ameishukuru Ofisi ya Kamishna wa Ardhi kwa kuanzisha kliniki hiyo, akieleza kuwa imemsaidia kupata hati yake kwa muda mfupi.
Aidha, amewahimiza wananchi wengine kujitokeza kupata huduma hiyo ili waweze kuthibitisha umiliki wao halali wa ardhi.
Kliniki hiyo inatarajiwa kutoa huduma kwa muda wa siku tano, huku wananchi wenye changamoto za ardhi na wanaohitaji hati za viwanja vyao wakihimizwa kufika katika eneo la huduma ili kupata msaada wa kitaalamu.