Wananchi waomba ujenzi wa daraja la Godegode na Kimagai
11 November 2026, 16:53

Ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya usafiri na mawasiliano kati ya Kata za Godegode na Kimagai, huku ukitarajiwa kurahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa maeneo hayo.
Na Steven Noel.
Wakazi wa Kata za Godegode na Pwaga, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa daraja linalounganisha Kata ya Godegode na Kimagai, wakieleza kuwa kukosekana kwa daraja hilo kunaendelea kuwa kikwazo katika shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa maeneo hayo.
Wakizungumza na Taswira ya Dodoma FM, baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamesema daraja hilo lina umuhimu mkubwa katika kurahisisha usafiri na mawasiliano kati ya kata hizo, huku wakieleza kuwa hali ya sasa imekuwa ikiathiri shughuli za maendeleo na kuwapa wananchi wakati mgumu wanapohitaji kusafiri kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kila siku.
Wameongeza kuwa changamoto hiyo huwa kubwa zaidi wakati wa msimu wa mvua, ambapo maji yanapoongezeka husababisha mawasiliano kati ya maeneo hayo na makao makuu ya Wilaya ya Mpwapwa kukatika, hali inayoweza kuwazuia wananchi kupata huduma muhimu kwa wakati, ikiwemo huduma za afya na shughuli nyingine za kijamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, George Nathan Malima, amesema anatambua changamoto hiyo inayowakabili wananchi na kueleza kuwa Serikali tayari imepata mkandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja hilo, hatua inayotoa matumaini ya kuondokana na changamoto ya mawasiliano inayojitokeza katika maeneo hayo.