Dodoma FM

Jamii yasisitizwa umuhimu wa kuendelea kulinda mazingira

11 August 2026, 17:05

Picha ni Mkurugenzi Mtendaji waThubutu Africa Initiatives na Mratibu Mkuu wa Jukwaa la Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Jonathan Kifunda akiongea katika jukwaa hilo.Picha na Anwary Shaban.

Jukwaa hilo limekuwa fursa kwa wadau wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kubadilishana uzoefu kutoka maeneo mbalimbali nchini, kujadili changamoto zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati ya pamoja ya kulinda mazingira.

Na Anwary Shaban.

Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa changamoto inayogusa maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, huku wadau wa mazingira wakisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kulinda mazingira .

Hayo yameelezwa jijini Dodoma, ambapo wadau wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekutana katika Jukwaa la Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, kwa lengo la kujadili changamoto zinazolikabili taifa pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji waThubutu Africa Initiatives na Mratibu Mkuu wa Jukwaa la Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Jonathan Kifunda, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa umewakutanisha wadau mbalimbali kujadili kwa pamoja hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Picha ni Jukwaa la Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi,lililofanyika jijini Dodoma leo hii.Picha na Anwary Shaban.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Agrith Forum na mmoja wa waandaaji wa jukwaa hilo, Isaya Sirungwe, amesema wadau wa mazingira wana wajibu wa kuhakikisha kila mwananchi anapata haki ya kuishi katika mazingira salama, safi na yanayolindwa.

Naye mmoja wa wadau kutoka maeneo mbalimbali waliohudhuria mkutano huo, Peter Mwamani, amesema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuonekana kupitia shughuli mbalimbali za kibinadamu, ikiwemo shughuli za uchimbaji wa madini.

Sauti ya Anwary