Wananchi watakiwa kuendelea kushiriki utunzaji wa mazingira
30 June 2026, 17:04

Shughuli hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuhamasisha jamii kushiriki katika utunzaji wa mazingira, kuongeza uoto wa asili na kujenga.
Na Anwary Shaban.
Mkuu wa Kitengo cha Mali Asili na Mazingira katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Happiness Karugaba, amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kuhakikisha maeneo wanayoishi yanakuwa safi na salama.
Karugaba, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Alhaji Jabir Shekimweri, ametoa wito huo wakati wa shughuli za kijamii zilizohusisha usafi wa mazingira na upandaji wa miti 40 katika Shule ya Msingi Kaloleni, zilizowakutanisha viongozi, wadau mbalimbali na wananchi wa Jiji la Dodoma.
Amesema utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na kwamba ushiriki wa jamii katika shughuli hizo unasaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko pamoja na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kariakoo Derby Tree, Richard Ole-Oosembe, amewashukuru wadau na wananchi wote walioshiriki katika zoezi hilo, akisisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unahitaji ushirikiano wa kila Mtanzania bila kujali nafasi yake katika jamii.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka Ngumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nikson Kimaro, ametoa shukrani kwa wadau waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo la usafi na upandaji miti, huku akitoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono kampeni ya usafi inayobebwa na kaulimbiu isemayo, “Mita tano usafi wangu, usafi wangu mita tano.”