Dodoma FM

Wanaume wahimizwa kufanya vipimo saratani ya tezi dume

27 July 2026, 16:59

Saratani ya tezi dume inaweza kusababishwa na sababu za kurithi.Picha na mtandao

Wananchi wameitaka serikali pamoja na wadau wa sekta ya afya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani ya tezi dume, wakiamini kuwa uhamasishaji wa mara kwa mara utasaidia kuongeza uelewa, kuondoa hofu ya kupima na kuwezesha wagonjwa wengi kugundulika mapema na kupata matibabu stahiki.

Na Daniel Njau.

Wananchi, hususan wanaume, wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini mapema saratani ya tezi dume, hatua itakayosaidia kupata matibabu kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo.

Akizungumza kuhusu ugonjwa huo, Daktari Hasroni Chuwa amesema saratani ya tezi dume inaweza kusababishwa na sababu za kurithi, ambapo mwanaume mwenye historia ya ugonjwa huo katika ukoo wake huwa na uwezekano mkubwa wa kuupata.

Ameongeza kuwa dalili zake ni pamoja na kuvimba kwa tezi dume na kuziba kwa njia ya mkojo, hali inayoweza kusababisha ugumu wa kukojoa na matatizo mengine ya mfumo wa mkojo.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu saratani ya tezi dume na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

 Hata hivyo, wameahidi kwenda kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kujikinga na tatizo hilo.

Simulizi na Daniel Njau