Wapambaji kucha watakiwa kuzingatia kanuni za afya
12 August 2026, 17:38

Wataalamu wa afya wamewasisitiza umuhimu wa usafi katika maeneo ya utoaji huduma za urembo, wakieleza matumizi ya vifaa safi na vilivyotakaswa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi na kulinda afya za wananchi.
Na Grace Budodi.
Wadau wa huduma za upambaji kucha jijini Dodoma wametakiwa kuzingatia usalama wa afya za wateja wao, huku wakisisitiza umuhimu wa usafi wa vifaa vinavyotumika ili kuzuia maambukizi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya vifaa visivyo safi.
Wakiongea na Taswira ya Habari, baadhi ya wapambaji kucha wamesema wameweka utaratibu wa kusafisha na kutakasa vifaa wanavyotumia mara baada ya kumhudumia kila mteja kabla ya kuvitumia tena kwa mteja mwingine, hatua wanayosema inalenga kulinda afya za wateja wao na kuhakikisha huduma zao zinakuwa salama wakati wote.
Kwa upande wake, mmoja wa wateja wa huduma za upambaji kucha amesema kabla ya kuhudumiwa huhakikisha vifaa vyote vinavyotumika vimesafishwa vizuri ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya vifaa visivyo safi.
Hata hivyo baadhi ya wateja wanasema wameamua kutumia vifaa vyao binafsi wanapokwenda kupata huduma za upambaji kucha kwa hofu ya kushirikiana vifaa na watu wengine, jambo wanaloamini linaongeza usalama wa afya zao.