Wanaume Dodoma wahimizwa kuvunja ukimya dhidi ya ukatili
9 June 2026, 18:06

Hata hivyo, amebainisha kuwa bado mwitikio haujafikia kiwango kinachotarajiwa, hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wanaume kuvunja ukimya ili kupata msaada na haki zao kwa wakati.
Na Elizabeth Tanzania.
Wanaume mkoani Dodoma wamehimizwa kuwa wazi na kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili ili kupata msaada kwa wakati na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Afisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Michael Mkinda, amesema bado kuna wanaume wengi wanaoshindwa kuripoti matukio ya ukatili kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo hali ya kisaikolojia inayowafanya kuogopa kuwashirikisha wengine changamoto wanazopitia.
Mkinda amesema mtazamo hasi uliopo kwa baadhi ya wanaume kuhusu kuripoti vitendo vya ukatili umekuwa ukichangia kuongezeka kwa madhara mbalimbali, ikiwemo changamoto za afya ya akili, msongo wa mawazo, na katika baadhi ya matukio kupoteza maisha, ambapo hali hiyo pia huathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema elimu inayoendelea kutolewa na Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na wadau mbalimbali imeanza kuleta matokeo chanya, ambapo idadi ya wanaume wanaofunguka na kuripoti matukio ya ukatili imeongezeka.