Ukatili wa kijinsia unakwamishaje elimu ya mtoto wa kike?
31 July 2026, 17:22

Jamii na wadau mbalimbali ni muhimu kushirikiana katika kumlinda mtoto wa kike na kumpa mazingira salama ya kusoma, kukua na kutimiza ndoto zake, huku wakisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha mtoto wa kike anapata fursa sawa ya kujenga mustakabali wake.
Na Daniel Njau.
Mila potofu na ukatili wa kijinsia katika jamii ni miongoni mwa sababu zinazowazuia watoto wa kike kutimiza ndoto na malengo yao, hasa katika jamii zinazoamini kuwa mtoto wa kike anapaswa kuolewa badala ya kupewa fursa ya kuendelea na masomo na kujijenga kwa maisha ya baadaye.
Akizungumzia hali hiyo, mwanasheria Bi. Eddah Mariki amesema mtazamo wa baadhi ya wanajamii unaochukulia ndoa kama hatima ya mtoto wa kike unaweza kumfanya kukatisha masomo yake, kupoteza fursa za maendeleo na kushindwa kufikia malengo aliyokuwa amejiwekea katika maisha.
Kwa upande wao, wanajamii wamesema wataendelea kuungana na kushirikiana katika kuhakikisha mtoto wa kike analindwa dhidi ya changamoto mbalimbali, zikiwemo ndoa za utotoni, ukatili na vitendo vingine vinavyoweza kuathiri maisha na maendeleo yake.