Migogoro ya familia yaweza kuathiri maendeleo ya watoto
25 September 2026, 16:36

Wito umetolewa na mkuu wa dawati la jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, ASP Christer Kayombo,akisisitiza wazazi umuhimu wa familia kuwa mazingira salama kwa watoto, ili kuwawezesha kukua katika malezi bora na kuendelea na masomo bila vikwazo vinavyoweza kutokana na migogoro ya kifamilia.
Na Anwary Shabani.
Imeelezwa kuwa kutengana kwa wazazi katika familia kunaweza kusababisha mabadiliko makubwa kwa watoto, ikiwemo kuathirika kisaikolojia, kitabia na kushuka kwa kiwango cha ufaulu shuleni.
Wakiongea na taswira ya habari baadhi ya Wazazi katika mtaa wa Mwatano wamesema migogoro na kuvunjika kwa familia kunaweza kumuathiri mtoto kutokana na mabadiliko ya mazingira ya malezi na maisha ya kila siku.
Wazazi hao wameongeza kuwa, baadhi ya watoto wanaweza kuonesha mabadiliko ya kitabia na kupoteza mwelekeo katika masomo, hali ambayo wanaeleza inaweza kuathiri maisha na mustakabali wao.
Akizungumza kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, ASP Christer Kayombo, amewataka wanandoa kulinda na kuthamini ndoa zao kwa kuepusha migogoro, akieleza kuwa watoto wanaweza kuathirika endapo familia itavunjika.
ASP Kayombo amesisitiza umuhimu wa wazazi kutanguliza ustawi na usalama wa watoto wakati wa kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika familia.