Polisi Dodoma yaimarisha operesheni za usalama barabarani
16 November 2026, 16:34

Jeshi la Polisi limeendelea kusisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja, huku madereva, makondakta na wamiliki wa vyombo vya usafiri wakitakiwa kuzingatia sheria na kuweka mbele usalama wa abiria badala ya maslahi binafsi.
Na Anwary Shabani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limeongeza kasi ya operesheni za ukaguzi wa vyombo vya moto, likilenga kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani vinavyohatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kubainika kwa makosa mbalimbali katika operesheni iliyofanyika katika baadhi ya mabasi ya abiria yanayo fanya safari zake nyakati za usiku ambapo mabasi hayo yalikutwa na makosa ya kubeba abiria zaidi ya idadi inayoruhusiwa.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, SSP Yusuph Kamota, amesema operesheni hiyo imebaini basi lililokuwa limebeba abiria ambao ni wanafunzi waliolazimika kukaa chini licha ya kulipa nauli, huku kondakta akiendelea kukusanya fedha bila kuwapatia abiria hao nafasi za kukaa.
Kutokana na hali hiyo, SSP Kamotta aliagiza wanafunzi waliokuwa ndani ya basi hilo kushushwa, kondakta kurejesha nauli walizolipa huku dereva akichukuliwa hatua kwa kukiuka taratibu za usafirishaji wa abiria.