Dodoma FM

Wananchi Bumira wamelalamikia umbali wa hospitali ya wilaya

23 October 2026, 16:45

Picha ni Hospitali ya wilaya ya bumita wilayani mpwapwa mkoani Dodoma. Picha na Dodoma fm.

Upatikanaji wa huduma za afya karibu na makazi ya wananchi ni muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu, hasa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka. Hata hivyo, umbali mrefu kutoka maeneo ya makazi hadi vituo vya afya unaweza kuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi, kutokana na gharama za usafiri na muda wanaotumia kufuata matibabu.

Na Stephen Noel.

Wananchi wa Kijiji cha Bumira, Kata ya Lupeta, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, wanalazimika kusafiri umbali wa kilomita 18 hadi 20 kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, hali inayowapa usumbufu na kuongeza changamoto ya kupata matibabu kwa wakati.

Wananchi hao, Jimmery Mwigune na Yese Magawa, wamesema umbali huo unawaathiri zaidi wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka, hivyo wameiomba Serikali na mamlaka husika kuimarisha huduma za afya zilizo karibu na makazi yao.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lupeta, Sospiter Mdokhono, amesema changamoto hiyo imeanza kufanyiwa kazi kupitia ujenzi wa kituo cha afya katika makao makuu ya kata, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakazi wa eneo hilo.

Wananchi wanatarajia kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza umbali wa kufuata matibabu na kuwawezesha kupata huduma za afya kwa urahisi na kwa wakati.

Hali hiyo inaibua umuhimu wa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo ya vijijini ili kila mwananchi aweze kupata matibabu kwa wakati bila kukabiliwa na changamoto kubwa za usafiri.

Simulizi na Stephen Noel.