Tanzania inatarajia utoshelevu wa chakula wa asilimia 130 kufikia 2025/2026
27 August 2026, 16:45

TPHPA itaendelea kushirikiana na Serikali, wakulima, vijana, wanawake, wafanyabiashara, watafiti pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ikiwemo zisizo za Serikali, kuhakikisha udhibiti wa visumbufu unaimarishwa na Tanzania inakuwa na kilimo chenye tija na uzalishaji endelevu.
Anwar Shabani,
Tanzania imeendelea kuimarika katika uzalishaji wa chakula, huku kiwango cha utoshelevu wa chakula kikifikia asilimia 130 katika mwaka wa 2025/2026, kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji pamoja na hatua mbalimbali za kudhibiti visumbufu vya mazao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, TPHPA, Profesa Joseph Nunguru, amesema hayo akiwa katika Ofisi ya Idara ya Habari Maelezo, iliyopo Mtumba jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchango wa mamlaka hiyo katika kulinda mazao.
Amesema katika kipindi hicho, Tanzania ilizalisha tani milioni 23 za chakula, huku TPHPA ikichangia mafanikio hayo kupitia udhibiti wa visumbufu vya mazao, ikiwemo magonjwa na wadudu wanaoweza kusababisha uharibifu na kupunguza uzalishaji.
Profesa Nunguru amesema katika kukabiliana na baa la panya, mamlaka hiyo ilifanya udhibiti katika mikoa sita, wilaya 13, kata 392 na vijiji 14,122, hatua iliyosaidia kuokoa jumla ya ekari 73,136 za mazao.