Dodoma FM
Dodoma FM
4 May 2026, 15:52

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetekeleza wajibu wake wa kuandaa eneo kwa kushirikiana na kamati, na kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa ufafanuzi kuhusu sakata la wafanyabiashara wa soko la Rehema Nchimbi baada ya eneo hilo kufungwa, ikibainisha kuwa ilichukua hatua mbalimbali kuwapatia maeneo mbadala ya kuendelea na shughuli zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 4,2026 Jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, amesema kuwa Halmashauri ilipokea taarifa ya kufungwa kwa soko hilo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma baada ya malalamiko ya wafanyabiashara kukosa maeneo ya kufanyia biashara.
Amesema kuwa Halmashauri ilipendekeza masoko mbadala yakiwemo Job Ndugai, Tambukareli, Makole na Kikuyu Kusini, ambayo yalikuwa na uwezo wa kuwachukua wafanyabiashara hao takribani 297, lakini wakayakataa wakidai hayakuwa mwafaka kwa shughuli zao.
Ameongeza kuwa baada ya mchakato huo, kamati ilipendekeza wafanyabiashara hao kuhamia eneo la Umonga lililopo mtaa wa Kitenge, kata ya Majengo, ambalo lina ukubwa wa mita za mraba 8,621 na ni eneo la kimkakati kibiashara.
Pia ameeleza kuwa Baada ya kamati kukamilisha kazi yake ilitoa mapendekezo kuwa wafanyabiashara hao wapatiwe eneo lililopo Mtaa wa Kitenge, Kata ya Majengo. Eneo hilo lipo kati ya Block Namba 43, Plot Namba 44 upande wa kaskazini na Block Namba 45 upande wa kusini ni eneo la wazi. Eneo linaukubwa wa mita za mraba 8,621.
Na kwa upande wake Nsubisi Kapula ambaye ni mkuu wa Divisheni viwanda biashara na uwekezaji ameleza kuwa watawaita viongozi wa soko kuweza kujadiliana juu ya mustakabali wa soko hili ikishindikana hatua za kisheria zichukuliwe.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetekeleza wajibu wake wa kuandaa eneo kwa kushirikiana na kamati, na kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara kuweza kutekeleza majukumu yao baada ya kukamilisha taratibu za kupitia rasimu ya mkataba na kuusaini. Aidha, halmashauri itaendelea kusimamia maelekezo ya waziri mkuu aliyoyatoa kuhusu uendeshaji wa eneo la Umonga. Zoezi la mwisho litakuwa ni ugawaji wa maeneo kwa ajili ya wafanyabishara hao kufanyia biashara.