Sekta za umma na binafsi zimetakiwa kushirikiana kuharakisha maendeleo
29 July 2026, 17:05

Mhe. Senyamule amesema usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora ni nguzo muhimu zitakazochochea maendeleo ya Mkoa wa Dodoma na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Na Anwary Shabani.
Viongozi na watumishi wa umma wametakiwa kubadili mitazamo yao kuhusu sekta binafsi na kuitambua kama mshiriki muhimu katika kuharakisha maendeleo ya uchumi na kufanikisha dira ya taifa ya maendeleo 2050.
Hayo yamesemwa na mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule,wakati akifunga kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Mkoa wa Dodoma kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.
Kikao hicho kilijadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Senyamule amesema maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha sekta binafsi inapewa mazingira rafiki ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa, hususan kwa kuwawezesha wawekezaji wa ndani ili Watanzania waweze kumiliki na kunufaika na uchumi wa nchi yao.
Aidha, amezielekeza halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha zinakamilisha kwa wakati miradi yote ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora, akibainisha kuwa bado kuna changamoto katika maendeleo ya vijiji, ikiwemo utekelezaji wa vikao vya vijiji ambao umefikia wastani wa asilimia 70.