Dodoma FM

Wananchi watakiwa kulinda vyanzo vya maji

17 September 2026, 17:08

Wananchi wameendelea kupewa elimu ya kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji ili kunusuru vyanzo hivyo. Picha na Dodoma fm.

Hata hivyo, jamii inapaswa kuendelea kushirikiana na mamlaka zinazohusika katika kulinda vyanzo vya maji na miundombinu yake, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mapema kuhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa maji, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Na: Mathias Mgale

Mchango wa wananchi katika kulinda na kuhakikisha usalama wa mifumo na vyanzo vya maji umetajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa maji salama na endelevu kwa jamii.

Wananchi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji, kutunza miundombinu ya maji pamoja na kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa vyanzo hivyo.

Baadhi ya wananchi wanasema ushiriki wao ni muhimu katika kuhakikisha vyanzo vya maji havichafuliwi, miundombinu haiharibiwi na maji yanatumika kwa uangalifu.

Wamesema jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa kuhusu uvujaji wa mabomba, uharibifu wa miundombinu, utupaji wa taka katika maeneo ya vyanzo vya maji pamoja na shughuli nyingine zinazoweza kuhatarisha upatikanaji wa maji salama.

Akizungumza kuhusu mchango wa wananchi katika kuhakikisha usalama wa mifumo ya vyanzo vya maji, Katibu msaidizi idara ya maji Kwamtoro Kondoa Bi. Zainabu Omary amesema usalama wa maji unahitaji ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka zinazohusika.

Amesema wananchi wana jukumu la kulinda mazingira yanayozunguka vyanzo vya maji, kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uchafuzi na kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanapoona changamoto katika mifumo ya maji.

Ripoti ya Mathias Mgale.