Dodoma FM

TACAIDS kujumuisha watu wenye ulemavu mapambano dhidi ya UKIMWI

28 August 2026, 16:10

Salali ameipongeza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania TACAIDS, kujumuisha walemavu mapambano dhidi ya UKIMWI. Picha na Ramla Kimu.

Kampeni hiyo inalenga kuwafikia watu wenye ulemavu wengi zaidi na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya UKIMWI, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya Tanzania katika kudhibiti ugonjwa huo yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi. Ameongeza kuwa juhudi za kupambana na UKIMWI zinapaswa kuwa jumuishi, ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika kupata elimu, taarifa na huduma muhimu za afya.

Na Ramla Kimu.                                                

Watu wenye ulemavu nchini wametakiwa kushirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, VVU, kwa kupewa elimu, taarifa sahihi na huduma za afya zinazozingatia mahitaji yao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Disabilities Hope, FDH, Maiko Salali, wakati akizungumzia umuhimu wa ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika programu na mikakati ya kitaifa ya kudhibiti UKIMWI.

Salali ameipongeza Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, TACAIDS, kwa juhudi inazozifanya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika mapambano hayo, akieleza kuwa kundi hilo ni sehemu ya jamii na halipaswi kuachwa nyuma katika upatikanaji wa elimu na huduma za afya.

Amesema TACAIDS imekuwa ikishirikisha watu wenye ulemavu katika programu mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu VVU na UKIMWI, jambo ambalo amesema limewasaidia kupata nafasi ya kushiriki katika juhudi za kitaifa za kudhibiti maambukizi.

Kwa upande wa FDH, Salali amesema shirika hilo limepanga kuendesha kampeni maalumu inayojulikana kama “NA SISI TUPO”, kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii, hususani watu wenye ulemavu na vijana, kuhusu umuhimu wa kupima afya, kujikinga na VVU pamoja na kuchukua hatua za kulinda afya zao.

Sauti na Ramla Kimu.