Wananchi Zaidi ya 5,000 Nala Waanza Kunufaika na Mradi wa Maji wa Bilioni 1.6
2 June 2026, 17:38

Mradi huo wa maji safi na salama unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya Nala na vitongoji jirani, huku ukiimarisha afya za wananchi, shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.
Na Mwandishi wetu.
Wananchi 5,188 wa maeneo ya Nala Center, Segu Juu, Chihoni pamoja na Kiwanda cha Mbolea cha Nala Itracom katika Jiji la Dodoma wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Uzinduzi huo umefanyika katika eneo la Nala ambapo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwan’gonda, amesema baada ya ukaguzi uliofanywa, mradi huo umebainika kutekelezwa kwa viwango vinavyokubalika na unalenga kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kuimarisha mazingira ya uwekezaji wa viwanda katika eneo hilo.
kiwasilisha taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Bernard Rugayi, amesema mradi wa maji safi na salama wa Kata ya Nala unahudumia maeneo yenye jumla ya wakazi 891,633 wa Wilaya ya Dodoma, huku ukiwa sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.
Mhandisi Rugayi ameongeza kuwa mradi huo unalenga kuboresha usambazaji wa maji na kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 88.4 kwa siku hadi kufikia lita milioni 91.2 kwa siku, hatua itakayosaidia kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi.
Naye Diwani leonard alexander wa Kata ya Nala amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, wananchi walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hali iliyowalazimu kutembea umbali mrefu kuyatafuta. Amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha hiyo na kuongeza ustawi wa wananchi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Nala wameiambia Dodoma TV kuwa ujio wa mradi huo ni mkombozi mkubwa kwao, wakieleza kuwa hapo awali walikuwa wakitumia muda mrefu na gharama kubwa kutafuta maji, tofauti na sasa ambapo huduma hiyo imewafikia karibu na makazi yao.