Dodoma FM

Wahitimu kidato cha sita waitwa JKT kwa mujibu wa sheria

28 May 2026, 17:30

Picha ni Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini, Meja general Rajabu Mabele,akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma.Picha na Maelezo.

Jeshi la Kujenga Taifa limetoa rai kwa vijana wote waliochaguliwa kuhakikisha wanafanya maandalizi mapema na kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya tarehe husikaa ambayo ni kuanzia tarehe 1-7 juni.

Na Mariam Kasawa.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini, Meja general Rajabu Mabele, ametoa wito kwa vijana wote waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026 kutoka shule za Tanzania Bara na Visiwani kujitokeza kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe mosi Juni hadi saba Juni mwaka 2026 kwa ajili ya kuanza mafunzo rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Mafunzo hayo yatatolewa katika makambi mbalimbali ya JKT nchini yakiwemo Ramkoma JKT, Msange JKT, Ruvu JKT pamoja na Kibiti JKT na makambi mengine yaliyotengwa kwa ajili ya mafunzo hayo.

Aidha, vijana wenye ulemavu wa kuonekana pamoja na wenye changamoto za viungo wametakiwa kuripoti katika kambii ya Ruvu JKT ambayo imeelezwa kuwa na miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwahudumia.

Sauti ya Meja general Rajabu Mabele,

Jeshi hilo pia limeeleza kuwa orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, makambi waliyopangiwa pamoja na vifaa vinavyotakiwa kupelekwa kambini vinapatikana kupitia tovuti rasmi ya JKT;

Sambamba na hilo, waombaji wametakiwa kupakua faili la “JKT PDF 2026” lililopo upande wa juu kulia wa ukurasa wa tovuti hiyo ili kuona majina yote pamoja na makambi waliopangiwa.