Dodoma FM

Mixx by Yas yaimarisha ushirikiano na vyama vya ushirika

6 July 2026, 17:49

Hafla hiyo imewakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika, hatua ambayo itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo.Picha na Anwary Shaban.

Kampuni hiyo imeingia makubaliano na vyama vya ushirika kwani kampuni hii imekuwa mdau wa TCDC Kwa  muda mrefu.

Na Anwary Shaban.

Kampuni ya Mixx by YAS Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano na vyama vya ushirika nchini kwa kusaini hati ya makubaliano itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanachama wa vyama hivyo.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa Biashara wa MIXX by YAS, James Sumari, ambapo amesema kampuni hiyo imeingia makubaliano na vyama vya ushirika kwani kampuni hii imekuwa mdau wa TCDC Kwa  muda mrefu.

Makubaliano hayo yamesainiwa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yanayo adhimishwa mwaka huu  yakiwa yamebeba kaulimbiu isemayo “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani.”

Akizungumza mara baada ya utiaji saini huo, Sumari amesema hafla hiyo imewakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika, hatua ambayo itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo.

Aidha, Sumari amesema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, zaidi ya wakulima laki tatu wameunganishwa kwenye huduma za kifedha kupitia mifumo ya MIXX by YAS, huku zaidi ya shilingi bilioni 700 zikilipwa katika sekta ya kilimo kupitia huduma hizo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msoffe, amesema thamani ya biashara iliyofanyika kupitia vyama vya ushirika nchini imefikia takribani shilingi trilioni 4.97, jambo linaloonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa taifa.

Sauti ya Anwary Kina.

Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yameendelea kusisitiza umuhimu wa ushirika katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku wadau wakihimizwa kuendelea kushirikiana ili kuongeza fursa za kifedha na maendeleo kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini.