Elimu ya malezi yatajwa kuwa msingi wa familia imara
28 July 2026, 16:57

malezi bora ni wajibu wa jamii nzima, wakisisitiza ushirikiano kati ya wazazi, walezi, shule na jamii kwa ujumla
Na Daniel Njau.
Wazazi na walezi wametakiwa kuimarisha ushiriki wao katika malezi ya watoto kwa kuhudhuria na kufuatilia vipindi vya malezi, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika kujenga jamii yenye maadili mema na watoto wenye tabia zinazokubalika.
Mtaalamu na msahuri malezi na Familia Bi, Sadaka Gandi , amesema malezi ni mchakato unaojumuisha mambo mengi yanayofanywa na mtu mzima ili kumwelekeza mtoto au kijana ambaye bado hajafikia umri wa kufanya maamuzi yake binafsi, hivyo akisisitiza umuhimu wa wazazi kuwa sehemu ya ukuaji wa watoto wao.
Kwa upande wao, wananchi wameeleza kuwa changamoto kubwa ya malezi inaanza pale wazazi wanapokosa muda wa kukaa na kuzungumza na watoto wao, huku jukumu hilo likiwaachwa zaidi wasaidizi wa kazi za ndani, hali inayoweza kuchangia kuporomoka kwa maadili.
Wananchi hao wameongeza kuwa malezi bora ni wajibu wa jamii nzima, wakisisitiza ushirikiano kati ya wazazi, walezi, shule na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yanayowajengea maadili mema na kuwafanya kuwa raia wema wa baadaye.