Dodoma FM

Shigela aagiza tathmini ya haraka bwawa la Dongobesh

25 September 2026, 17:06

Picha ni mwonekano wa bwawa la Dogobesh mkoani Manyara. Picha na Dodoma fm.

Hali ya bwawa la Dongobesh imeibua tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua kubwa, hivyo Serikali imeanza kuchukua hatua za kitaalamu kuzuia madhara kwa wananchi na miundombinu inayozunguka eneo hilo.

Na Kitana Hamis.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Martine Shigela, ameagiza wataalamu kufanya tathmini ya haraka ya Bwawa la Dongobeshi wilayani Mbulu, kufuatia hatari ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.

Ameagiza TANROADS, TARURA, Halmashauri pamoja na Serikali ya Mkoa kukamilisha tathmini hiyo ndani ya siku tatu, ili mahitaji ya kifedha yawasilishwe kwa Waziri wa Kilimo au Mkurugenzi Mkuu wa Umwagiliaji kwa hatua za kudhibiti maji na kulinda bwawa, barabara na madaraja.

Mhe. Shigela pia amewataka wananchi wanaoishi karibu na mabonde na njia za maji kuchukua tahadhari mapema na kutambua maeneo salama ya kuhamia endapo mvua zitaongezeka.

Amesema tayari kuna dalili za mmomonyoko katika njia ya maji, akisisitiza kuwa usalama na uhai wa wananchi ni muhimu zaidi kuliko mali.

Simulizi na Kitana Hamis.