Dodoma FM

Wanafunzi Ilolo kutembea umbali mrefu kwenda shule

29 October 2026, 16:40

Picha ni wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kuyafikia mazingira ya shule. Picha na mwananchi.

Kutokukamilika kwa ujenzi wa shule shikizi katika Kitongoji cha Ilolo, Kata ya Ihumwa jijini Dodoma, kumewalazimu wanafunzi kuendelea kutembea umbali mrefu kufuata huduma za elimu katika maeneo ya Ihumwa na Iyumbu.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa kitongoji hicho, kilichopo karibu na mpaka wa Iyumbu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamesema wanafunzi hulazimika kutembea kilomita kadhaa kufika shuleni. Wameeleza kuwa madarasa mawili yaliyoanzishwa kwa lengo la kupunguza changamoto hiyo yalipaswa kukamilika mwaka jana, lakini hadi sasa ujenzi wake haujakamilika.

Mwenyekiti wa Maendeleo wa Kata ya Ihumwa, Edward Magawa, amekiri kuwa eneo hilo linakua kwa kasi na kuongeza mahitaji ya vyumba vya madarasa katika shule zilizopo, pamoja na ujenzi wa shule mpya. Amesema wanaendelea kutafuta njia za kukabiliana na changamoto hiyo ili kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu kwa watoto wa kata hiyo.

Simulizi na Victor Chigwada.