Dodoma FM

Wataalam wahimiza umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana

15 October 2026, 17:20

Picha ni Kijana na mtaalamu wa Afya akipewa elimu kuhusu afya ya uzazi. Picha kutoka Instagram.

Elimu ya afya ya uzazi kwa vijana inatajwa kuwa nyenzo muhimu katika kujenga uelewa, kuimarisha afya na kuwawezesha vijana kufanya maamuzi yenye manufaa kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Na Anwary Shabani.

Wito umetolewa kwa jamii kuendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wa jinsia zote mbili ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao, kuepuka mimba za utotoni na kufikia malengo yao ya maisha.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Elizabeth Festo, mwezeshaji wa elimu ya rika kutoka Shirika la Restless Development, lililopo Chamwino mkoani Dodoma, kupitia Mradi wa Kijana Imara, akieleza kuwa afya ya uzazi inahusisha ustawi wa kimwili, kiakili na kijamii katika masuala yanayohusiana na mfumo wa uzazi.

Aidha, Festo amesema vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 wanapaswa kupata elimu ya afya ya uzazi ili kuwawezesha kujitambua, kufanya maamuzi sahihi na kujikinga na changamoto mbalimbali za kiafya.

Amefafanua kuwa huduma za afya ya uzazi zinapatikana katika vituo vya afya, ambako vijana wanaweza kupata huduma rafiki zinazotolewa kwa usiri na bila hofu ya kuhukumiwa na watoa huduma, hatua inayoweza kuwahamasisha kujitokeza kupata ushauri na huduma zinazohitajika.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Dodoma wameeleza maoni yao kuhusu wajibu wa wazazi katika kuwapatia vijana elimu ya afya ya uzazi, huku wakibainisha changamoto zinazoweza kuwazuia vijana kupata elimu hiyo.

Simulizi na Anwary Shabani.