Dodoma FM

Wananchi miyuji waungana kufanya usafi wa mazingira

5 October 2026, 17:17

Picha ni wananchi wa kata ya miji wakifanya usafi kwa pamoja ili kutunza mazingira. Picha na Anwary Shabani.

Zoezi hilo limeendelea kuwa sehemu ya hamasa kwa wananchi kushiriki katika usafi wa mazingira, hasa katika maeneo ya mabonde na maeneo mengine yanayoweza kukusanya maji, ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

Na Anwary Shabani.

Wananchi wa Kata ya Miyuji, Mtaa wa Matias, eneo la Hado jijini Dodoma, wamejitokeza kufanya usafi kwa kushirikiana na Green Samia Foundation, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuweka mazingira safi, kuzuia magonjwa ya mlipuko na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na mkusanyiko wa maji wakati wa mvua.

Usafi huo umefanyika katika eneo linalotajwa kuwa na uwezo wa kukusanya maji mengi, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kushirikiana na Serikali na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi na salama.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Green Samia Foundation, Mahfoudh Haji, amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama.

Mahfoudh amesema wamefika katika Mtaa wa Matias baada ya kubaini kuwa eneo hilo linahitaji usafi wa haraka kutokana na kuwa bonde linaloweza kukusanya maji mengi, hali ambayo inaweza kusababisha madhara endapo mazingira hayataandaliwa mapema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Green Samia Foundation, Injinia Ruben Chacha, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kushiriki katika usafi huo kupitia mradi wa Walk and Pick, kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali na viongozi katika kulinda usafi wa mazingira.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Miyuji, Seleman Mazengo, amesema wananchi katika Mkoa wa Dodoma wamekuwa wakishiriki kufanya usafi kila Jumamosi, huku akiwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kushiriki katika usafi na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wake, Balozi wa Mtaa wa Matias ameishukuru Green Samia Foundation kwa kushirikiana na wananchi katika zoezi hilo, huku baadhi ya wananchi wakisema taasisi hiyo imewaunga mkono kwa kuwapatia vitendea kazi vya usafi na hivyo kuongeza nguvu katika juhudi za kuweka mazingira safi.

Simulizi na Anwary Shabani.