Dodoma FM

Maonesho ya parachichi kuimarisha kilimo cha kisasa na tija kwa wakulima

13 October 2026, 10:44

Picha ni Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Ngambila akitembelea baadhi ya madanda katika maonesho hayo. Picha na BUSOKELO.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza uelewa kuhusu afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kukuza ushirikiano kati ya wakulima na wadau wengine ili kuongeza uzalishaji na manufaa ya zao la parachichi kwa wakulima na uchumi wa eneo hilo.

Na Mwandishi wetu.

Wakulima wa zao la parachichi wametakiwa kutumia fursa za maonesho ya parachichi yanayofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya kujifunza mbinu za kisasa za kilimo zitakazoongeza uzalishaji na tija pamoja na kuboresha kipato chao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya.

Picha ni Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Ngambila akitia saini katika moja ya mabanda ya maonesho aliyopita. Picha na BUSOKELO.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho hayo, Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Ngambila aliyemwakilisha Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu kwa wakulima kupata elimu na teknolojia za kisasa zitakazowasaidia kuzalisha parachichi bora na kuongeza thamani ya zao hilo.

Sauti ya Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Ngambila

Katika hatua nyingine, Afisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mushoborozi Christian ameeleza kuwa maonesho hayo yatawasaidia wakulima kufahamu faida na umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa parachichi, ikiwemo kuboresha afya ya udongo na kuongeza ubora wa mazao.

Sauti ya Afisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Mushoborozi Christian

Kwa upande wake, mkulima wa zao la parachichi Prisca Butuyuyu amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo, akisema kuwa yana nafasi kubwa ya kuongeza uelewa na mwamko kwa wakulima kujikita katika uzalishaji wa parachichi wenye tija, huku akibainisha umuhimu wa kuendelea kuandaa majukwaa yatakayowaunganisha wakulima na wadau mbalimbali wa zao hilo.