Dodoma FM

Ukatili wa kijinsia wakwamisha ndoto za mtoto wa kike

6 October 2026, 11:56

Pichani mtoto wa kike anaelazimishwa kufanyiwa ukatili wa kingono. Picha na mwananchi.

Jamii imetakiwa kuacha vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto wa kike, ikiwemo kuwaozesha katika umri mdogo, kwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuwanyima fursa ya kupata elimu, kuathiri afya yao ya akili na mwili, pamoja na kuwazuia kutimiza ndoto na malengo yao ya maisha.

Na Daniel Njau

Ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, hususan wasichana, umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowakwamisha kutimiza ndoto zao, kutokana na athari za kisaikolojia na kimwili zinazoweza kujitokeza baada ya kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa vitendo hivyo bado vinaendelea katika jamii, ikiwemo kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo, hali inayowafanya baadhi yao kukatisha masomo na kushindwa kufikia malengo yao ya maisha.

Mtaalamu wa saikolojia, Bi Eddah Mariki, amesema jamii inapaswa kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanalindwa na kupata haki zao, ikiwemo haki ya elimu, ili waweze kukua katika mazingira salama na kutimiza ndoto zao.

Amesema jamii haipaswi kunyamazia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto au kuvimaliza kifamilia, bali inapaswa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kulinda haki na mustakabali wa watoto.

Simulizi na Daniel Njau