TANESCO yawapatia majaji elimu ulinzi wa miundombinu ya umeme
28 August 2026, 16:38

Kiobya amewaomba watumishi hao kutumia uelewa walioupata kusaidia kukomesha hujuma na uharibifu wa miundombinu ya umeme, huku akihimiza matumizi ya nishati safi, ikiwemo kupikia kwa kutumia umeme na matumizi ya vyombo vinavyotumia umeme katika shughuli mbalimbali.
Watumishi wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wasajili, Mahakimu, Watendaji na wafanyakazi wengine, wamefanya ziara katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Mtera kwa lengo la kujifunza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wananchi.

Akizungumza Agosti 27, 2026 wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Huduma za Usalama wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lenin Kiobya, amesema jumla ya watumishi 59 wa Mahakama walishiriki ziara hiyo, ambapo walipata uelewa kuhusu mchakato mzima wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu ya maji pamoja na shughuli zinazofanywa na TANESCO.
Kiobya amesema ziara hiyo inalenga kujenga mahusiano na ushirikiano mzuri kati ya TANESCO na Mahakama, hasa katika utekelezaji wa majukumu ya kisheria yanayohusu miundombinu ya umeme. Amesema uelewa huo utasaidia katika tafsiri ya sheria na kuzingatia maslahi ya taifa pale Mahakama inaposhughulikia kesi zinazohusiana na miundombinu ya umeme na hujuma dhidi yake.