Zimamoto yaitaka jamii kutumia kwa usahihi namba ya dharula na uokoaji
15 June 2026, 16:16

Kwa mujibu wa majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji yaliyoainishwa chini ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Sura ya 427, wananchi wanapaswa kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa huduma za uokoaji na kukabiliana na majanga katika jamii.
Na Elizabeth Tanzania.
Jamii mkoani Dodoma imetakiwa kutumia kwa usahihi namba ya dharula ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 114 kwa ajili ya kuripoti matukio ya dharura yanayohitaji msaada wa haraka, badala ya kuitumia kwa mambo yasiyohusiana na huduma hiyo.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Afisa Habari, Uhusiano, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Msaidizi (ASF) Steven Kate amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia namba hiyo kuomba vocha za simu na hata kuwapigia wahudumu kwa lengo la kuwatongoza, jambo ambalo ni kinyume na madhumuni ya huduma hiyo ya dharura.
Amesema namba 114 imeanzishwa mahsusi kwa ajili ya kupokea taarifa za matukio ya dharura ikiwemo majanga ya moto, ajali za barabarani pamoja na matukio mengine yanayohitaji huduma za uokoaji, tofauti na masuala ya jinai yanayoshughulikiwa na vyombo vingine vya usalama.
Aidha, ASF Kate amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa wakati pindi wanapobaini tukio la dharura ili kuwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika eneo la tukio mapema na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Ameongeza kuwa jeshi hilo lina jukumu la kulinda maisha na mali za wananchi kupitia huduma za uzimaji moto, uokoaji na utoaji wa elimu ya kinga dhidi ya majanga mbalimbali.