Kampeni ya mjue jirani kukomesha uhamiaji haramu
12 August 2026, 17:07

Baadhi ya wananchi wameendelea kusisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhamiaji haramu hayawezi kuachwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi katika kutoa taarifa na kulinda usalama wa nchi.
Na Anwary Shabani.
Uhamiaji haramu umeendelea kuwa changamoto inayohitaji ushirikiano wa wananchi na vyombo vya dola, huku wananchi wakitakiwa kuwa macho na kutoa taarifa kuhusu watu wanaoingia au kuishi nchini kinyume cha taratibu za kisheria.
Taswira ya habari imezungumza na Mkaguzi wa Ofisi ya Uhamiaji, Dominic Adamu Wanna, ambapo amesema hati ya kusafiria, yaani passport, hutolewa kwa Mtanzania anayekidhi vigezo, huku akieleza kuwa kuna aina mbalimbali za hati hizo kulingana na mahitaji ya msafiri.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Ofisi ya Uhamiaji, Vincent Misana, amesema sheria imeweka adhabu kwa watu wanaohusika na makosa yanayohusiana na uhamiaji haramu, ikiwemo faini na kifungo, huku akisisitiza kuwa ulinzi wa nchi ni wajibu wa kila mwananchi.
Naye Polisi kata wa kata ya Miyuji ambaye pia ni afisa uhamiaji Yahaya Juma, amewataka wananchi kuendelea na kampeni ya mjue jirani yako kwa kujua watu wanaoishi katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanapobaini viashiria vya uhamiaji haramu.