Jamii yatakiwa kutambua ukeketaji ni kitendo cha hatari
15 July 2026, 17:59

Jitihada hizo zinaendelea kuonesha dhamira ya serikali na wadau mbalimbali ya kuhakikisha ukeketaji unatokomezwa kabisa, huku wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za elimu na kutoa taarifa za vitendo hivyo ili kulinda afya, haki na mustakabali wa mtoto wa kike.
Na Anwary Shaban.
Wananchi wametakiwa kuachana na mila potofu ya ukeketaji inayopelekea athari kwa wanawake na wasichana.
Kufuatia vitendo hivi kuendelea kwa siri katika baadhi ya jamii Wananchi wa kijiji cha Soya, Wilaya ya Chemba wanatarajiwa kupata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji pamoja na sheria zinazopiga marufuku vitendo vya ukeketaji katika mnada wa kijiji utakaofanyika Jumapili, Julai 19, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendelea kutokomeza ukeketaji mkoani humo Dodoma.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dodoma,Bi. Honorata Michael, amesema elimu hiyo itatolewa kwa wananchi wote watakaoshiriki mnadani ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya ukeketaji, haki za mtoto wa kike na malengo ya mkakati wa taifa wa kutokomeza vitendo vya ukeketaji.
Amesema Mkoa wa Dodoma bado una kiwango cha takribani asilimia 18 cha ukeketaji, hali inayohitaji ushirikiano wa wadau na jamii ili kukomesha jambo hilo.
Honorata amesema mbali na utoaji wa elimu, wananchi watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala ya ukeketaji, hatua zinazochukuliwa na serikali pamoja na taratibu za kisheria zinazowalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Chifu wa Mkoa wa Dodoma, Mtemi Emanuel Mazengo, amesema viongozi wa jadi wanaendelea kushirikiana na serikali kupambana na ukeketaji kwa kutoa elimu kwa jamii, kuwafikia mangariba wanaojihusisha na vitendo hivyo pamoja na kuunda kamati za kina mama zitakazosaidia kufuatilia na kuzuia ukeketaji katika ngazi ya jamii.
Aidha, Honorata Michael amekumbusha kuwa sheria ya mtoto, kifungu cha 13 Sura ya 160, inapiga marufuku ukeketaji, na kwamba mtu yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha kuanzia miaka mitano hadi miaka 15, au kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni mbili, au adhabu zote kwa pamoja.