Dodoma FM

Serikali yatoa tahadhari kwa wanaotoa ushauri wa lishe mtandaoni

20 May 2026, 11:36

Picha ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi.Picha na Bunge.

Hatua hizo zinalenga kulinda afya za wananchi dhidi ya upotoshaji wa taarifa zinazotolewa kupitia majukwaa ya kidijitali bila kuzingatia misingi ya kitaalamu.

Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inatambua ongezeko la watu binafsi na baadhi ya wataalamu wanaotoa elimu na ushauri wa afya pamoja na lishe kupitia mitandao ya kijamii bila kuwa na taaluma inayotambulika, hali inayoweza kuwapotosha wananchi na kuhatarisha afya zao.

Akijibu swali la Mbunge wa Hai, Mhe. Saasisha Elinikyo Mafuwe, bungeni jijini Dodoma Mei 19, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema changamoto hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa uelewa wa masuala ya afya na lishe, utandawazi pamoja na kukua kwa matumizi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Amesema Serikali inaendelea kudhibiti hali hiyo kupitia utekelezaji wa Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009, hususan kifungu cha 173(1), ambacho kinamtaka mtoa maudhui, mada au matangazo yanayohusu afya ya jamii kupata kibali kutoka kwa Waziri wa Afya au afisa aliyeidhinishwa.

Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali itaendelea kuelimisha wananchi kufuata ushauri wa afya kutoka kwa wataalamu wenye sifa na wanaotambulika ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu afya na lishe.

Pia Dkt. Samizi amesema hatua hizo zinalenga kulinda afya za wananchi dhidi ya upotoshaji wa taarifa zinazotolewa kupitia majukwaa ya kidijitali bila kuzingatia misingi ya kitaalamu.

Sauti ya Dkt. Samizi.