Serikali kutumia mafunzo ya ujasiriamali kutengeneza bidhaa
14 July 2026, 10:12

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani Morogoro, Beatrice Njawa, amesema mwandishi wa habari anaweza kuwa mtengenezaji wa bidhaa na mtumishi wa umma anaweza kuwa mjasiriamali na huo ndio mwelekeo wa taifa.
Na Mwandishi wetu.
Serikali imeahidi kuhakikisha washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Jukwaa Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) wanayafanyia kazi kwa vitendo kwa kuwawezesha katika mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zitakazochangia ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Morogoro na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Beatrice Njawa, wakati akifungua mafunzo hayo kwa wananchi.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayoratibiwa na Jukwaa huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) na kutolewa na wakufunzi wa taasisi ya MAMO ENTREPRNEURSHIP yanalenga kuwajengea wananchi mbalimbali uwezo wa kubuni miradi ya ujasiriamali itakayowaongezea kipato na kuchangia ajira kwa vijana.

Mbali na hayo Njawa amelipongeza JUWATA kwa kuona mbali na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda. “Habari peke yake haitoshi. Amesema kuwa Mwandishi wa habari anaweza kuwa mtengenezaji wa bidhaa na mtumishi wa umma anaweza kuwa mjasiriamali huo ndio mwelekeo wa taifa,” amesema Bi.Njawa.
Katika hatua nyingine Bi.Njawa ameeleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kupitia Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itafanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha washiriki wanatekeleza waliyojifunza na kuahidi kuwa vikundi vitakavyofanya vizuri vitapewa kipaumbele na mwakani 2027 watapelekwa katika maonesho ya Sabasaba.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa JUWATA wa kuwajengea wanachama wake uwezo wa kujitegemea kiuchumi sambamba na kutekeleza majukumu yao ya kuhabarisha umma.